Kwanini tunatakiwa kuwajibika kutokana hisia zetu kwenye mahusiano yetu?

Kwanini tunatakiwa kuwajibika kutokana hisia zetu kwenye mahusiano yetu?

Hisia zetu zina umuhimu sana kwenye maisha yetu. Kila hali unayoipitia kwenye maisha yako, hisia zako zimehusika. Uwe unajua au hujui. Mtu kukutukana tusi huwa haliwi tusi mpaka wewe utakavyolipokea. Mtu akikudharau wewe haiwi dharau mpaka utakapojidharau wewe, na kisha kuchochea hisia. Vile wewe utakavyolichukulia jambo, ndivyo hisia zitaanzia hapo kufanya kazi. Watu huwa hawafadhaishwi na vitu, bali na maoni wanayochukua wenyewe alisema Epectitus, akiweka msisitizo kwenye jambo hili.

Hisia zetu siku zote tunatakiwa tuzidhibiti na kuzitawala, na tunatakiwa kuwajibika pale tunaposhindwa kufanya hivyo. Tunatakiwa kufahamu kuwa, kile watu wanakisema na kukifanya dhiidi yetu kinaweza kikawa ni kichocheo, lakini siyo kisababishi cha hisia zetu au vile tunavyoweza kujisikia.

Hisia zetu mara nyingi huwa zinatokana na kile sisi tumechagua kukipokea kutokana na kile watu wanatusema na kutufanyia, lakini pia kutokana na mahitaji yetu na matarajio yetu kwa wakati huo. Kama mtu atakusema au kukufanyia kitu ambacho ni hasi na si cha kiungwana, unamachaguo manne ya namna utakavyo lipokea jambo hilo. 

Namna ya kwanza ni kulichukulia suala hilo kibinafsi, kwa kujilaumu na kupinga. Mfano, mtu anahasira na anakwambia “wewe ni mjinga sana”. Kwa haraka haraka na wewe unajiambia, mimi kweli ni mjinga, nilitakiwa nielewe hichi kitu. Maana yake utakuwa umelichulia suala hilo kibinafsi. Unakuwa umekubaliana na hukumu ya mtu mwingine juu yako, na unaanza kujihukumu na kujilaumu. Ukichagua njia hii, unakuwa umechagua kutokujithamini, na hivyo kuendelea kujisikia wewe ni mkosaji, kujisikia aibu na hata kusononeka.  

Namna ya pili unavyoweza kulipokea jambo ambalo ni hasi kwako na si la kiungwana ni kumpinga kumrudishia muhusika aliyekusema au kukutendea jambo hilo. Mfano kama amekwambia “wewe ni mjinga”, unampinga kwa kusema hapana, mimi siyo mjinga bali wewe ndiye mjinga. Hapa kinachofanyika ni kuwalaumu wengine. kwa kupokea jambo hili kwa namna hii unatengeneza au kuamsha hasira kwa pande zote mbili. 

Namna ya tatu ni kutambua hisia na mahitaji yetu. Pale tunapopokea ujumbe au jambo hasi, ni vizuri kufahamu hisia zetu na mahitaji yetu. Kama mtu amekuambia “wewe ni mjinga”. Unaweza kumjibu kuwa, unavyosema mimi ni mjinga, najisikia vibaya, kwani nahitaji kueleweshwa na kundishwa zaidi kwenye hili jambo. Kwa kuelekeza umakini wetu kwenye hisia zetu na mahitaji yetu kwa wakati huo, tunakuwa na ufahamu kuwa, tunavyojisikia kwa sasa kunatokana na uhitaji wa sisi kujifunza. 

Namna ya nne ya kupokea jambo hasi unayoweza kuitumia ni kutambua hisia na mahitaji ya wengine. Mfano kama mtu amekwambia “wewe ni mjinga” unaweza ukamuuliza unajisikia vibaya kwa sababu mimi nilitakiwa niwe na jua hiki kitu?, kwa kufanya hivyo unakuwa umeshafahamu hisia na hitaji lake kwako, kwamba ulitakiwa uweumejifunza kitu hicho ili usiwe mjinga, hivyo unakuwa unawajibika kutokana na hisia zako.

Rafiki, tunatakiwa tuwajibike kutokana na hisia zetu badala ya kuwalaumu wengine, kwa kutambua mahitaji yetu, shauku yetu, mategemeo yetu, maadili yetu na hata fikra zetu pia. Mfano, mtu anakwambia uliniangusha sana kwanini hukuja kwenye kwenye kikao chetu. Na mtu mwingine akakwambia, uliniangusha sana, kwanini hukuja kwenye kikao chetu? nilikuwa nimepanga nikupe zawadi yako.

Hapa mtu wa kwanza, anapeleka masikitiko yake moja kwa moja kwa mtu mwingine. Lakini mzungumzajiwa pili yeye anaonyesha chanzo cha masikitiko yake, ni hitaji au shauku yake ya kutoa zawadi ambayo haijatimizwa, hivyo anawajibika zaidi kwenye hisia na hitaji lake zaidi kuliko kuwalaumu watu wengine. 

Ukawe na siku njema rafiki, unapoendelea kutafakari hisia zetu na umuhimu wake kwenye mahusiano yetu. Pia ili kuendelea kupata makala hizi na huduma zetu kwenye emaili yako jiandikishe hapa chini.

Felician Meza

Mwandishi wa vitabu,

Mwalimu wa mafanikio

Mwanasayansi

© Felician Meza 2021

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *