Hii ndiyo nguvu ya shauku

Hii ndiyo nguvu ya shauku

Karibu rafiki kwenye tafakari yetu ya leo.

Kama ulipitwa na makala iliyotangulia soma hapa

Shauku ndiyo hisia inayozichochea hisia zingine ziweze kufanya kazi kwenye maisha yetu. Shauku ni kama kiu inayokuongoza uchukue hatua, iwe ni hatua hasi au chanya.  Ili uchukue hatua chanya, iruhusu hisia yako ya shauku ifuatiwe na hisia ya furaha. Kwani, shauku ni kichocheo tu, lakini furaha ndiyo inazitwala hisia zote iwe ni hisia chanya au hasi, furaha huzitawala zote. 

Kadri shauku yako juu ya jambo fulani inavyokuwa kubwa ndivyo ambavyo pia uwezekano wa kuchukua hatua kubwa unaongezeka. Nakumbuka mwaka 2013 nikiwa chuoni nilikutana na rafiki yangu ambaye aliniletea video za Dr. Myles Munroe na kuniambia nizisikilize. Baada ya kuzisikiliza, niliandika kwenye notebook yangu kuwa mtu huyu hatokufa mpaka nikutane naye. 

Ilikuwa mwaka 2014 nikiwa ndiyo nimemaliza masomo yangu ya chuo kikuu, nilipata taarifa kutoka kwa rafiki yangu kuwa Dr.Myles alikuwa anakuja Dar es salaam kwaajili ya semina na makongamano. Waandaaji wa shughuli ile walikuwa wameweka ghalama za kulipia kwenye semina hizo, hivyo nilijaribu kutafuta pesa, lakini sikufanikiwa kwani tiketi zilikuwa zinauzwa bei ya juu sana. Nakumbuka tiketi moja ilikuwa inauzwa dola mia tano.

Kwa kuwa shauku ya kukutana na Dr. Myeles ilikuwa kubwa sana, niliwaendea kamati ya maadalizi ya shughuli ile, na kuwaomba waweze kupokea kiwango kidogo nilichokuwa nacho. Baada kufanya kikao chao, waandaaji wa shughuli ile walikubali kupokea shilingi elfu hamsini tu ambayo ndiyo nilikuwa nayo. 

Mwenyekiti wa kamati ya maadalizi baadaye alikuja kuniambia kuwa walikubali kwa sababu waliona shauku yangu ilikuwa ni kubwa sana, hasa pale nilipo waonesha notibuku yangu ya mwaka 2013 pale nilipokuwa nimeandika kuwa lazima niona na Dr. Myles kabla hajafa. Wiki mbili baada ya kukutana naye pale Serena hoteli Dar es salaam kwenye semina yake na wafanyabiashara, nilipokea taarifa za kifo chake pamoja na mke wake, kwenye ajali ya ndege. Pamoja na hayo yote kutokea, tayari nilikuwa nimetimiza ndoto yangu ya kukutana naye kwa sababu shauku ndiyo ilikuwa ikinisukuma kuchukua hatua. 

Hisia hii ya shauku inanguvu sana, kwani ndiyo inakusukuma ufurahi, inakusuma ucheke, inakusukuma upende na inakusukuma ukasirike, uogope au uchukie. Mihemuko au hisia chanya ni mbili tu ambazo ni furaha na upendo, lakini lazima zisukumwe na shauku. Changamoto ni kuwa, shauku bila kuongozwa na furaha, itazalisha msukumo hasi pale inapokutana na hisia zile ambazo zinaweza kuhasiwa (yaani kutumika kuwa hasi) kama chuki, hasira, uoga au huzuni. 

Rafiki, unatakiwa kufuata mfumo huu; ili uweze kuzifanya hisia hasi ziwe chanya, na uzitumie kuchukua hatua muhimu kwenye mahusiano na maisha yako kwa ujumla.  Mfumo huu ni shauku, inatakiwa iichochee furaha, kisha furaha ndiyo izitawale hisia zingine. Kwa kufanya hivyo hutakuwa na hisia hasi, bali zitakuwa chanya. Mfano hisia ya hasira, ni nzuri sana kwani bila ya hiyo huwezi kuchukua hatua na kubadilika. Lakini ili usichukue hatua hasi, inatakiwa hasira itanguliwe na hisia ya furaha, ndipo hasira zako zitakuwa na faida badala ya hasara.

Ukawe na siku njema rafiki, unapoendelea kutafakari hisia zetu na umuhimu wake kwenye mahusiano yetu. Pia ili kuendelea kupata makala hizi na huduma zetu kwenye emaili yako jiandikishe hapa chini.

Felician Meza

Mwandishi wa vitabu,

Mwalimu wa mafanikio

Mwanasayansi

© Felician Meza 2021

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *